UCSAF YAKAMILISHA UJENZI WA MINARA 758; WANANCHI MILIONI 8.5 WANUFAIKA NA HUDUMA ZA MAWASILIANO
Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekamilisha kwa mafanikio ujenzi wa minara yote 758 ya mawasiliano ya simu kote nchini, hatua iliyowezesha kuanza kwa utoaji wa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti katika vijiji 1,407 vilivyopo kwenye kata 713 za mikoa yote ya Tanzania Bara, vijiji vyote hivyo awali vilikuwa havina huduma hizo.
Kupitia utekelezaji wa mradi huo, jumla ya wananchi takribani milioni 8.5 wameanza kunufaika na huduma bora za mawasiliano, hali inayorahisisha upatikanaji wa taarifa, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi, pamoja na kuongeza fursa katika sekta za elimu, afya, biashara na ajira, hususan kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini na pembezoni.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote bila ubaguzi.
“Kukamilika kwa ujenzi wa minara 758 ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika upatikanaji wa huduma za mawasiliano. Kupitia mradi huu, wananchi wamepata fursa mpya za kielimu, kiuchumi na kijamii, hususan walioko maeneo ya vijijini na pembezoni,” alisema Mhandisi Mwasalyanda.
Utekelezaji wa miradi ya mawasiliano nchini hufanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali kupitia UCSAF na watoa huduma za mawasiliano za simu nchini, ambapo Serikali hutoa ruzuku ili kuchochea uwekezaji katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara, huku watoa huduma wakitoa utaalamu wa kiteknolojia, ujenzi wa miundombinu na uendeshaji wa huduma.
Kupitia ushirikiano huo, kampuni ya Honora (Yas) imejenga minara 261, Vodacom Tanzania imejenga minara 190, Airtel Tanzania imejenga minara 169, Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imejenga minara 104, huku Halotel ikijenga minara 34, hatua iliyochangia kukamilika kwa jumla ya minara 758 ya mawasiliano ya simu kote nchini. Jumla ya ruzuku iliyotolewa na Serikali kupitia UCSAF kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ni shilingi bilioni 126.
Wananchi waliopo katika maeneo yaliyofikiwa na mradi huo wameeleza kuridhishwa kwao na maboresho ya huduma za mawasiliano. Hosiana Mwaiteleke, mkazi wa Kata ya Ifwenkenya mkoani Songwe, alisema kuwa kabla ya ujenzi wa mnara huo hali ya mawasiliano ilikuwa duni, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli za kibiashara katika eneo hilo.
“Hali ya mawasiliano ilikuwa mbaya sana kwa sababu eneo kubwa la biashara lilikuwa halina mtandao. Ujio wa mnara umetukomboa wafanyabiashara na kutatua changamoto kubwa ya mawasiliano tuliyokuwa nayo,” alisema.
Kwa upande wake, Besta Mashishi, mkazi wa Kijiji cha Ruchima, Kata ya Majimoto mkoani Katavi, alisema kuwa kabla ya ujenzi wa mnara walilazimika kupanda juu ya miti ili kupata huduma ya mawasiliano.
“Kabla ya mnara kujengwa tulikuwa na shida kubwa ya mawasiliano kiasi cha kulazimika kupanda juu ya miti ili kupata mtandao. Sasa hivi hata ukiwa nyumbani unapata mawasiliano vizuri,” alisema.
Naye Ahoso Sagdai, mkazi wa Kijiji cha Endamaghechan, Wilaya ya Karatu mkoani Manyara, alisema kuwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano umeleta mabadiliko makubwa, hususan katika nyakati za dharura.
“Awali ilikuwa vigumu sana kuwasiliana, hasa pale ulipokuwa na mgonjwa na unahitaji msaada wa haraka. Sasa huduma za mawasiliano zinapatikana kwa urahisi na zinatusaidia kuokoa muda na maisha,” alisema.
UCSAF itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inaendelezwa na kuboreshwa zaidi ili kufikia maeneo yote ambayo bado hayajapata huduma za uhakika, sambamba na azma ya Serikali ya kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu nchini.