WAZIRI KAIRUKI ASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MINARA 201 YA MAWASILIANO VIJIJINI
Serikali Yatoa Ruzuku ya Bilioni 19.7, Wananchi milioni 2.85 Kunufaika na Huduma
Ahimiza Ubora na Utekelezaji wa Haraka wa Miradi
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amewataka watoa huduma za mawasiliano nchini kuhakikisha kuwa miradi ya kufikisha mawasiliano vijijini inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vilivyokubalika, ili kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumza leo, tarehe 05 Desemba 2025, katika hafla ya utiaji saini mikataba ya Utekelezaji wa Mradi wa Mawasiliano ya Simu Vijijini – Awamu ya Kumi, kati ya UCSAF na watoa huduma za mawasiliano, Mhe. Kairuki ameshuhudia utiaji saini wa mradi wa minara 201 itakayogharimu shilingi bilioni 19.7 katika kata 201 zenye vijiji 263, utakaowanufaisha Watanzania milioni 2.85 wanaoishi vijijini.
Mhe. Kairuki amesema hatua hiyo ni muhimu katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2025/2030 pamoja na Dira na Mkakati wa Kitaifa wa Miaka 10 wa Uchumi wa Kidijitali.
Amesisitiza kuwa masharti ya mikataba lazima yaheshimiwe na kusimamiwa kama sheria, na utekelezaji wa mradi huo uzingatie ubora wa huduma pamoja na kukamilisha kazi kabla au ndani ya muda uliopangwa. Aidha, amewataka watoa huduma kutoa taarifa mapema pale wanapokutana na changamoto ili ufumbuzi upatikane haraka na wananchi waweze kupata mawasiliano kwa wakati.
Ameongeza kuwa tathmini ya upatikanaji wa mawasiliano inapaswa kuendelea kufanyika nchi nzima ili maeneo ambayo bado hayajafikiwa yaingizwe kwenye hatua zinazofuata za upanuzi wa miundombinu. Pia amesisitiza matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali kwa kufuata mifumo rasmi ili kuharakisha utekelezaji.